UCHAWI TATIZO LA DUNIA
Katika makala iliyotangulia tulijikumbusha kwamba Mwenyezi Mungu aliumba mitishamba kwa lengo la kumnufaisha mwanaadamu. Kwa hekima zake alimuumba mwanaadamu kutokana na udongo, ndani ya udongo huo akaweka kila aina ya madini yanayo hitajika katika mwili wa mwanaadamu ili kuujenga na kuulinda. Kadhalika tuliona uchawi ambao ni zao la shetani ulivyopata wafuasi dunia nzima na kuiathiri jamii ya mwanaadamu.
Katika sehemu hii tutaangalia kwa ufupi aina mbili za uchawi na unavyoandaliwa.
Kuna uchawi wa kila aina kulingana na eneo, kwa mfano katika nchi za Afrika uchawi umegawanyika katika sehemu kuu mbili, uchawi wa bara na uchawi wa pwani. Uchawi wa pwani ni tofauti na uchawi wa bara kwa sababu watu wa pwani walipata wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia, hasa Wazungu na Waarabu baadhi ya wageni waliwafundisha wenyeji uchawi mpya kabla na wao kujifundisha uchawi wa wenyeji.
Kabla hatujaona kwa muhtasari namna uchawi unavyoandaliwa, ni muhimu kuzingatia lengo la makala haya, sio kufundisha uchawi bali lengo hasa ni kujikumbusha namna wachawi wanavyohangaika tena kwa gharama na muda mwingi kuisumbua jamii ya wanaadamu, na nini kifanyike kuweza kuishinda hila yao.
Ni ukweli ulio wazi kwamba huwezi kumshinda adui yako kijeshi kama haufahamu aina ya silaha alizonazo, idadi ya askari wake na uhodari wao pamoja na nguvu za kiuchumi. Nataraji iwapo utajua uchawi unavyoandaliwa na unavyo muathiri mwanaadamu utajiweka vizuri kupambana nao, na utakuwa mwepesi kung'amua kwa urahisi viashiria vya uchawi.
Ni muhimu kuelewa kuwa hakika uchawi upo wala sio habari za kubuniwa. Kadhalika ni muhimu kukumbuka kuwa mchawi hakimbiwi, wala sio sawa ule usemi usemao kuwa mchawi mpe mtoto amlee, ni kweli akimlea hawezi kumdhuru lakini atamuandaa ili awe mshirika wake.
Kuna maelfu ya aina za uchawi duniani na tutazitaja polepole kadri tutakavyo pata muda. Hapa tutataja uchawi wa kifungo na faraka, uchawi wa kifungo huandaliwa kwa ajili ya kumfunga mwanaadamu asifanikiwe katika maisha yake, kwa uchawi huu mwanamke hufungwa ili asiolewe na mwanaume asioe, aidha mwanaume anaweza kufungwa ili asiweze kumjamii mkewe, pia mwanamke anaweza kufungwa ili asipate ujauzito au ashindwe kujifungua. Kadhalika uchawi wa kifungo huandaliwa ili kumzuia mtu asipate kazi, akilima asifanikiwe, asisome na hata anapo soma asielewe.
Vilevile upo uchawi wa faraka ( mfarakano), uchawi huu huandaliwa ili kumtenganisha wanaadamu na jamii inayomzunguka, tunafahamu mshikamano ndio nguvu kuu ya harakati yeyote katika jamii, aliyepatwa na uchawi huu anaweza kutengwa na mumewe au mkewe hili likitokea ndoa huvunjika, mtu anaweza kufarakana na mkuu wake wa kazi na kazi ikakoma, kwa uchawi huu unaweza kutengwa na wateja ukajikuta kutwa nzima unasinzia wakati wenzako wanafanya biashara. Aidha unaweza kutenganishwa na watoto wako wa kuzaa, nao watoto wanaweza kutengwa na wazazi wao wakati bado wanahitaji usaidizi kutoka kwao.
Uchawi wa kifungo huandaliwa kwa miti mitano, kuna sehemu nyingine miti huongezwa au kupunguzwa itategemea. Huenda miti nitakayo itaja hapa ikawa na majina tofauti katika sehemu nyingine. Mti wa kwanza ni mzizi wa mti wowote unaokatisha njia (mpindula nzila), mti mwingine unaitwa mtaizi, mkaangwele, mlalilwefii na mfulukilizya. Kumbuka anaye wezesha uchawi kufanya kazi ni shetani mwenyewe, kazi anayofanya mchawi ni kumsogeza au kuandaa mtandao utakaowezesha shetani aweke nguvu zake katika dawa ili iwe uchawi.
Katika uchawi huu wa kifungo na faraka, vifaa kadhaa huandaliwa ambavyo huchanganywa katika dawa, vifaa hivyo ni pamoja na inzi, nyuki na wadudu waliojifia, kinyesi cha mbwa, paka na kinyesi cha binaadamu asiyefahamika.
Mchawi akifika katika mti unaoitwa mtaizi ambao ndio mkubwa kwa uchawi wa aina hii kwanza huvua nguo zake kisha huuzungushia mti huo majivu huku akisema maneno maalumu, halafu huchimba mizizi kwa kubana pumzi anapoingia katika duara na kisha huiachia pumzi anapotoka nje ya duara, akisha chimba na kupata mizizi hujisadia kinyesi juu ya mizizi kisha huvunjia juu yake yai viza (yai bovu), halafu hufukia mchanga na kuondoka. Baada ya siku saba hurudi katika mti huo alfajiri akiwa na kifaranga mweusi.
Akifika huvua nguo zake na husema maneno maalumu, halafu hufukua akisha ipata mizizi huchinjia kifaranga mweusi kisha hukata mizizi na kuigeuza, kifaranga hufukiwa pale na kuondoka na mizizi. Mizizi hiyo huchanganywa na ile mizizi ya miti mingine tuliyoitaja, kisha husangwa na kupata unga na kuwekwa katika kopo jeusi kisha hulipeleka kopo hilo makaburini usiku saa sita.
Akifika makaburini huvua nguo na kubaki kama alivyo zaliwa, kisha hupiga hodi mara tatu na kujikaribisha mwenyewe, hapo kazi ya kumwita shetani kwa maneno maalumu hufululiza. Baadaye huenda katikati ya makaburi na kuchimba shimo na kufukia kopo na kuondoka. Baada ya siku 21 hurudi akiwa na zawadi maalumu ambayo huiacha pale alipolifukia kopo, kisha hukuchukua kopo na kwenda nalo.
Mpaka hapo umeshaona sumu yenye mionzi mikali inavyo sukwa. Ni muhimu kukumbuka kwamba makaburini baadhi ya majini, misukule na mashetani wameweka makazi yao huko, kazi iliyofanywa tangu mwanzo ni kuandaa mazingira yatakayo wezesha kumchukua shetani ili waweze kuishi ndani ya dawa husika. Mtu aliye logwa na uchawi huo anaweza kuweweseka kama mtu aliyepagawa na pepo.
Dalili nyingine anaweza kuota akiwa makaburini au kumuota mtu mweusi, paka mweusi au kibwengo, anaweza kuota akimjamii mtoto wake wa kike aliye mzaa au mama yake mzazi, na kwa mwanamke mfano kama huo. Kadhalika anaweza kuota amefukiwa ndani ya shimo jeusi mno, au amevaa nguo nyeusi, aidha anaweza kuota amejikojolea kitandani.
Dawa iliyopo ndani ya kopo tiyari ni sumu yenye mionzi mikali, mchawi anapo lishika kopo tu shetani husogea haraka kusikiliza maelezo ili aweze kufanya kazi inayo hitajika.
Kwa dawa hiyo utafukuzwa kazi, au wewe mwenyewe utaandika barua ya kuacha kazi, na utawakimbia wote wataonyesha nia ya kutaka kukusaidia. Kwa dawa hiyo utamuandikia mkeo talaka wakati bado unampenda, au mkeo atafunga virago yeye mwenyewe kwa swala dogo lisilokuwa na msingi, kwa mwanamke atakataa kila aina ya wachumba, na mwanaume atawaona wanawake ni maadui zake, kwa dawa hiyo utajikuta jela baada ya kuhusushwa na tukio ambalo hulifahamu, aidha kutokana na uchawi huo unaweza kupatwa hasira na ukachukua uamuzi wa kuyafupisha maisha yako kwa sababu za kipuuzi kama wivu wa mapenzi, na unaweza kuamka asubuhi ukiwa mzima ukapatwa na ajali yenye utata ukajikuta ukiishi maisha yaliyobakia ukiwa mlemavu.
Jambo muhimu ambalo mimi na wewe yatupaswa tuliweke akilini, ni kwamba uchawi haumuathiri mtu aliyejisogeza vya kutosha kwa Mwenyezi Mungu, na anapo patwa na uchawi ni rahisi kutibiwa kwa wakati. Tunaomba utuandikie kwenye comment nini fikra yako kuhusu tatizo hili la uchawi ili wasomaji makini waweze kukuza uelewa wao kuhusu jambo hili.
POINTI hizi zinahitaji majibu. Namna gani mtu analogwa? Na uchawi unaanza kumuathiri mtu kwa muda gani? Je kuna tofauti gani kati ya mwanga na mchawi? Mtu akiwa mchawi anaweza kuacha, kama ndio nini kifanyike? Kweli lambalamba (kamchape) huwanyang'anya watu uchawi? Mtu anaweza kulogwa aonekane kuwa ni mchawi wakati sio mchawi? Mtu mwenyewe akiwa nyumbani afanye nini ili kujitibu uchawi na kujikinga?
Nakusihi tukutane katika makala ijayo.
0621270517.
Comments